Chasambi azungumzia sababu za kuwekwa benchi Simba
Winga chipukizi wa Simba, Ladack Chasambi, awatoa hofu mashabiki kuhusu kuwekwa benchi
Ladack Chasambi, winga wa Klabu ya Simba, amewatoa hofu mashabiki baada ya kusema kuwa kukaa kwake benchi ni sehemu ya kujifunza kutoka kwa wachezaji wakubwa. Aliahidi kwamba siku moja atapata nafasi ya kudumu, akisisitiza kuwa hakuna mchezaji anayeweza kupata namba kirahisi bila kuipambania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Chasambi, ambaye alisajiliwa msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, alisema ni kawaida kwa mchezaji kujisikia vibaya kukosa nafasi ya kucheza. Hata hivyo, alisisitiza kuwa nafasi inahitaji jitihada na sio tu kupewa.
Mchezaji huyo alijibu malalamiko ya mashabiki wengi kuhusu kutopata nafasi ya kucheza, huku Kocha Mkuu, Fadlu Davids, akimpa Joshua Mutale nafasi zaidi. Chasambi alionyesha heshima kwa Mutale, akisema ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu ambaye anajifunza mambo mengi kutoka kwake.
“Ushindani ni mkubwa sana Simba na ni kawaida kwenye klabu za mpira. Unapaswa kupigania namba popote unapoenda. Nimekuwa nikisikia maneno kuhusu Mutale, lakini kwa upande wangu, naona ni mchezaji mzuri na ninajifunza kutoka kwake,” alisema Chasambi.
Kuhusu hisia zake za kukaa benchi, Chasambi alikiri kuwa ni kawaida kujisikia vibaya, lakini hiyo inampa motisha ya kufanya vizuri zaidi katika mazoezi ili kumshawishi kocha. “Ni lazima upambane ili upate nafasi. Mashabiki wasiwe na wasiwasi, nitacheza tu, na tuzingatie kwamba sote tunaipambania timu moja,” aliongeza.
Wakati Chasambi akizungumza, klabu hiyo pia imemsajili winga mwingine, Elie Mpanzu, ambaye anatarajiwa kujiunga na timu katikati ya Desemba mwaka huu. Mpanzu, ambaye ana uzoefu wa kimataifa, atazidisha ushindani wa nafasi kwenye kikosi hicho, kwani pia ni miongoni mwa mawinga wenye uwezo wa kufunga mabao.