E NEWS

TPLB yapiga faini Coastal Union na kuwapa onyo Yanga

Katika hatua ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeipiga faini Klabu ya Coastal Union na kuonya Yanga kwa makosa ya kuchelewa kufika uwanjani.

Katika taarifa iliyotolewa jana, TPLB ilisema Yanga imepewa onyo kali kwa kuchelewa kufika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kwa mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC, ambao waliushinda kwa bao 1-0 tarehe 29 Septemba mwaka huu.

TPLB ilifafanua kuwa Yanga ilifika uwanjani saa 1:48 usiku, wakati ilipaswa kuwa huko saa 1:30 usiku, kwa mujibu wa Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kulingana na Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu.

Klabu ya Coastal Union pia imepewa faini ya Sh. milioni moja kwa kuchelewa kuwasilisha orodha ya wachezaji na maofisa wa ufundi kabla ya mchezo wao dhidi ya Mashujaa FC, uliochezwa tarehe 13 Septemba mwaka huu, Uwanja wa KMC Complex, ambapo walifungwa bao 1-0. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.

Coastal Union pia imepewa onyo kwa kuchelewa kuwasilisha orodha ya wachezaji na benchi la ufundi kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC tarehe 29 Agosti, ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Timu hiyo iliwasilisha orodha saa 7:50 mchana, badala ya saa 7:00 mchana, kama ilivyoelezwa katika Kanuni ya 17:6, na adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.

Kwa upande mwingine, Tabora United imepigwa faini ya Sh. milioni moja kwa kushindwa kujumuisha wachezaji angalau wawili wa timu za vijana kwenye kikosi chao katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KenGold, ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Kamati hiyo ilisema Tabora United imerudia kosa hili katika michezo minne licha ya kukumbushwa mara kadhaa.